Katibu wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma Bw. Kubingwa Mashaka Simba amesema kuna umuhimu wa kuziimarisha ofisi za Wilaya za Watu Wenye ulemavu kwa kupatiwa huduma bora wanazostahiki.
Akikabidhi Muundo wa Taasisi kwa Baraza la Taifa la watu wenye ulemavu na Mfuko wa huduma za Afya Zanzibar na Muundo wa Utumishi kwa Tume ya Ukimwi Zanzibar huko Ofisini kwake Mwanakwerekwe Bw. Kubingwa amesema muundo huo umezitambua ofisi hizo kwa vile zinahudumia kundi muhimu hivyo utekelezaji wa sera na Sheria uzitambue ofisi za Wilaya kwa lengo la kuziimarisha.
Amesema lengo la serikali kurekebisha miundo ya Taasisi na ile ya utumishi sio kwa ajili ya maslahi pekee bali ni kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa Wananchi.
Hivyo amewaomba wakuu wa Taasisi kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wa miundo yao ili kuongeza kasi ya uwajibikaji kwa watumishi wa umma.
Naye Katibu mtendaji wa Baraza la Taifa la watu wenye ulemavu Bw Ussi Khamis Debe ameishukuru serikali kwa kuwajengea heshima na hadhi watu wenye ulemavu.
Kwa Upande wake Kaimu Mkurugenzi Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar ZHSF Bw Yassin Ameir Juma akipokea muundo huo ameahidi kwenda kusimamia utekelezaji wake kwa lengo la kuimarisha huduma za Afya.
Mapema Mkurugenzi Idara ya Miongozo na uchambuzi Miundo Kutoka Kamisheni ya Utumishi wa Umma Bw. Kharib Khamis Mustapha amesema baada ya kukabidhi Miundo kamisheni hiyo Hufanya Ukaguzi kwa taasisi za Umma ili kuangalia utekelezaji wake.