Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeridhia miundo mipya ya Taasisi ya Mhasibu mkuu wa Serikali na Mamlaka ya Serikali za mitaa ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa Wananchi.
Akikabidhi miundo hiyo kwa Taasisi hizo huko ofisini kwake Mwanakwerekwe Katibu wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma Ndg. Kubingwa Mashaka Simba amesema utekelezaji wa haraka wa miundo hiyo utaleta mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi wanaowatumikia.
Ndg. Kubingwa amewahimiza wakuu wa Taasisi hizo kwenda kusimamia ipasavyo utekelezaji wa miundo hiyo ili kufikia matarajio ya Serikali ya kuondoa changamoto ya Kiutendaji na utoaji wa huduma.
Amesema lengo la miundo hiyo sio kwa ajili ya maslahi pekee bali ni kuimarisha uwajibikaji kwa watendaji kwa kuzingatia sifa za kielimu na kiutumishi.
Wakipokea miundo hiyo Mhasibu mkuu wa Serikali Nd. Hamad Saleh Hamad na Mkurugenzi utumishi na Uendeshaji katika Ofisi ya Rais, Twala za mikoa Ndg. Silima Juma Khamis wameishukuru Serikali kwa maamuzi yake ya kupitisha miundo hiyo kwani itaongeza kasi kwa watumishi wao kufanyakazi kwa bidii na kuiahidi Serikali kuongeza kasi ya utoaji huduma
.
Mapema Mkurugenzi Miongozo na Uchambuzi wa Miundo kutoka Kamisheni ya Utumishi wa Umma Ndg. Gharib Khamis Mustafa amesema kazi ya ushughulikiaji wa miundo hiyo imechukua muda mrefu kutokana na umuhimu wake kwa jamii na Taifa.