Katibu wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma Ndg. Kubingwa M. Simba amezitaka Bodi za Taasisi za Umma kuijuilisha Kamisheni hiyo Changamoto zinazojitokeza hasa katika Masuala ya Kiutumishi.
Nd Kubingwa ameyaeleza hayo wakati akikabidhi Miundo ya Taasisi kwa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Taasisi ya Wahasibu na Baraza la Sanaa, sensa na Filamu (BASSFU) ofisini kwake Mwanakwerekwe.
Amesema ni Jukumu la Kamisheni hiyo kuhakikisha inasimamia Utumishi hapa Zanzibar hivyo bodi hizo zinapaswa kuwasiliana na kamisheni kwa ajili ya kupatiwa maelekezo na ushauri wa kitaalamu katika masuala ya Kiutumishi.
Amefahamisha kuwa Bodi hizo pia ni sehemu ya Kusimamia Utumishi wa Umma kama ilivyo Tume zote za Utumishi ambazo ni Tume ya Utumishi ya Baraza la Wawakilishi,Tume ya Utumishi ya Mahakama, Tume ya Utumishi ya Idara maalum za SMZ na Tume ya Utumishi Serikalini.
Amefahamisha kuwa Kamisheni hiyo itaendelea kuyafanyia kazi kwa ufanisi mkubwa mapendekezo ya Taasisi za Umma yanayowasilishwa kwa ajili ya kuimarisha Miundo yao kabla ya kuwasilishwa Serikali kuu kwa ajili ya kuidhinishwa na Serikali kuu.
Ameishukuru Serikali kwa kuwa sikivu kwa kuridhia Miundo hiyo hatua ambayo ni utekelezaji wa Utawala bora.
Ndg. Kubingwa ameeleza kuwa usimamizi wa Miundo hiyo ni hatua muhimu ya kuimarisha Utendaji na Utoaji wa Huduma kwa Umma.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bi Rukia Hamad Abdalla akitoa Shukurani zake Kwa kukabidhiwa Muundo amesema jukumu lao ni kwenda kuusimamia ili kutimiza malengo ya Serikali ya Kuimarisha Utumishi wa Umma.