MAWASILIANO KATIKA SEHEMU ZA KAZI & MAMBO YA KUZINGATIA KATIKA UKAGUZI WA RASILIMALI WATU

Wafanyakazi wa Kamisheni ya Utumishi wa umma wametakiwa kuongeza kasi ya uwajibikaji na ufanisi hasa katika suala zima la kufanya ukaguzi  na uchunguzi katika Taasisi za umma.

Kauli hiyo imetolewa na  mkuu wa Divisheni ya Ukaguzi Kutoka Kamisheni hiyo Nd, Rehama N. Khamis, wakati akitoa mada ya Muongozo  wa Ukaguzi katika mafunzo ya ndani kwa watendaji wa Afisi kuu ya Kamisheni yaliyofanyika Mwanakwerekwe,  tarehe 7 Agost,2024.

Amesemamafunzo hayo yatasaidia wakaguzi na wadau wa ukaguzi kupata uelewa na kurahisisha utekelezaji wa zoezi la Ukaguzi  kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na muongozo huo ili kufanikisha kazi  ya ukaguzi

Amefahamisha kuwa Lengo kuu la Uchunguzi na Ukaguzi ni kutathmini kwa kiwango gani Mamlaka za Ajira, Nidhamu na Waajiri wanazingatia Sera, Sheria, Kanuni na taratibu za usimamizi wa rasilimaliwatu

Amefahamisha kuwa kazi ya ukaguzi wa rasilimali watu ina umuhimu mkubwa kwani ina lengo la Kutathmini hali ya uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo  Pamoja na Kuonesha mafanikio na mapungufu katika kusimamia Rasilimali watu katika Utumishi wa Umma.

Hivyo amesema ni jukumu la Mamlaka za Ajira, Mamlaka za Nidhamu na Waajiri Kutoa vielelezo vinavyotakiwa na Timu ya Uchunguzi na Ukaguzi Pamoja na Kumuandaa Afisa atakayesaidia Timu ya Uchunguzi na Ukaguzi kutoka Kamisheni ya utumishi wa umma ili kufanikisha kazi hiyo ya Ukaguzi.

          Pia ni muhimu Mamlaka hizo Kuwapa taarifa watumishi watakaohitajika kuhojiwa na muda watakaotakiwa kwa kazi ya Ukaguzi na Kuhakikisha usalama wa Wakaguzi kwa muda wote katika eneo la ukaguzi.

Naye Afisa utumishi kutoka Kamisheni hiyo Bw. Ame J. Khatibu, Akiwasilisha mada kuhusu Mkataba wa utoaji  huduma  kwa  umma  amesema katika uongozi wa kisasa huduma zinatakiwa  kutolewa kwa haraka  na  kwa  ufanisi kwa mujibu wa mkataba huo.

          Amefahamisha kuwa Lengo la mkataba huo wa huduma kwa umma ni kutoa muongozo kwa wataka huduma na wadau wengine katika kutoa huduma za Kamisheni na kujenga ushirikiano katika kazi kwa ajili ya kutoa huduma bora.

Ameongeza kuwa wataka huduma hao wanapaswa kuelewa huduma hizo zitatolewa kwa namna gani na muda wa kutolewa huduma wanazozihitaji.

          Aidha amesema kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa Kamisheni hiyo ni kuwa, Tume za Utumishi, Wizara na Taasisi zote za SMZ, Mashirika ya umma wakala Tendaji na wananchi kwa ujumla ni wataka huduma wao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *