Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Katiba Sheria,Utumishi na Utawala bora Mhe Haroun Ali Suleiman amesema ni jukumu la Wakuu wa taasisi na vitengo kukaa pamoja kujadili namna ya kuwaelimisha watendaji wao juu ya utekelezaji wa sheria ya Utumishi wa Umma
Akizungumza katika Mkutano wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma Zanzibar na taasisi zinazojitegemea na wakala Tendaji wa SMZ huko Ukumbi wa Bima Mperani Mhe Haroun amesema Serikali imeweka Sheria na Kanuni bora za Utumishi lakini tatizo ni kushindwa kuzitafsiri na kuzitekeleza ambpo wafanyakazi wengi hufanyakazi kwa Mazowea bila kuzielewa Sheria hizo.
Amesema pamoja na jitihaha zinazochukuliwa na Serikali bado kuna malalamiko kwa baadhi ya watumishi kutowajibika ipasavyo na kuchelewa kufika kazini,kutoka bila ya dharura zinazokubalika kwa mujibu wa sheria na kanuni za Utumishi wa Umma.
Amefahamisha kuwa mambo hayo ndio yanayorudisha Nyuma jitihada za Serikali za kutoa huduma bora na kwa haraka kwa wananchi na kudhoofisha jitihada Serikali za kuimarisha Uchumi wa Nchi.
Hivyo Mhe Haroun amesema ni matumai yake kuwa mkutano huo utasaidia kuondoa baadhi ya Kasoro hizo kwa kwenda kusimamia na kuzifahamu taratibu za kisheria za Utumishi.
Naye Katibu wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma Kubingwa Mashaka Simba amesema Kamisheni hiyo i imeshafanya mkutano kama huo kwa Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi kwa lengo la Kusimamia na kuimarisha Utawala bora na Sekta ya Utumishi wa Umma.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ukaguzi Rufaa na malalamiko kutoka kamisheni ya Utumishi wa Umma Bi Asya Mussa Ali, amesema baadhi ya kasoro zilizobainika katika taasisi za umma ni kuwa taarifa za Watumishi kutohifadhiwa katika mfumo wa Kielektronic hivyo amewataka wakuu wa Taasisi kuitumia mifumo inayowekwa na Serikali ili kwenda Sambamba na Malengo yanayowekwa
Wakichangia Washiriki wa Mkutano wameomba taarifa za Ukaguzi wa Watumishi wa Umma ziwekwe wazi ili kuimarisha Uwajibikaji kwa Watumishi hao kwa taasisi zao.
Mkutano huo ulioandaliwa na Kamisheni ya Utumishi wa Umma umewashirikisha Wakuu wa Taasisi, wenyeviti na makatibu wa bodi za Taasisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.