Kamisheni ya Utumishi wa umma imesema utekelezaji wa muundo wa utumishi wa Kampuni ya Mwani Zanzibar utaleta mageuzi katika kutoa huduma kwa wananchi.
Akikabidhi muundo huo kwa Uongozi wa Kampuni ya Mwani huko ofisini kwake Mwanakwerekwe Katibu wa Kamisheni ya Utumishi wa umma Ndg. Kubingwa Mashaka Simba amesema muundo huo utaimarisha uwajibikaji kwa kuzingatia sifa za kielimu na kiutumishi.
Hivyo Bw Kubingwa amewahimiza viongozi wa Kampuni hiyo kusimamia ipasavyo utekelezaji wa muundo huo ili kufikia matarajio ya Serikali ya kuondoa matatizo ya kiutendaji na utoaji wa huduma.
Hata hivyo Bw Kubingwa amesema Kamisheni ya Utumishi wa Umma imeridhishwa na utekelezaji mzuri na wa haraka wa muundo wa Taasisi hali iliyosababisha kukabidhiwa Miundo wa Utumishi.
Amesema Kuna taasisi 57 zimeshakabidhiwa miundo ya Taasisi lakini ni chache tu zilizokwisha kamilisha miundo ya utumishi ikiwemo Kampuni ya Mwani
“Leo ninakwambieni kuwa kuna taasisi 57 tumeshazikabidhi miundo ya Taasisi lakini ni chache zilizokamilisha miundo ya utumishi mukiwemo nyinyi Kampuni ya mwani kwa kweli mmefanya kazi kubwa” alisema
Akipokea muundo huo Mkurugenzi Rasilimali watu Mipango na utawala wa Kampuni ya Mwani Zanzibar Nd. Mwadini Makame Haji ameahidi kuusimamia na kuutekeleza ili kuimarisha utoaji wa huduma.
Amesema Kampuni hiyo itaendelea kuimarisha huduma na soko la mwani kwa wakulima wa zao hilo ili kwenda sambamba na sera ya serikali ya kuimarisha uchumi wa buluu.
Amefahamisha kuwa azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Dk Mwinyi ni kuona sekta ya Uchumi wa buluu inaimarika, Hivyo ameishuku Kamisheni ya Utumishi wa umma kwa kufanikisha upatikanaji wa muundo huo.