Mkurugenzi Idara ya Utawala Rasilimali watu na mipango kutoka Kamisheni ya Utumishi wa umma Ndg Maryam Rished Mbarouk amesema mafunzo yanayotolewa kwa watendaji wa taasisi hiyo yatasaidia kuwajengea uwezo na uelewa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi.
Akizungumza katika mafunzo kwa watendaji hao huko Mwanakwerekwe, Amesema ni jukumu la kila mfanyakazi kuelewa muundo wa taasisi yake uongozi , wakuu wa Divisheni na dhamana wanazokabidhiwa na majukumu yake ya kila siku.
Mkurugenzi huyo amefahamisha kuwa ikiwa watafanya hivyo basi majukumu ya Kamisheni ya utumishi wa Umma yatatekelezwa kwa ufanisi mkubwa.
Naye Mkuu wa Divisheni ya Miundo ya Mawizara Wakala Tendaji na Mashirika ya Umma Bw. Muhsini Ame Ali Akitoa mada Katika mafunzo hayo kuhusiana na Muundo wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma amesema faida kuu ya muundo wa Taasisi ni kuwa na mgawanyo uliowazi wa majukumu.
Aidha amesema Muundo wa Taasisi hujumuisha mambo muhimu ikiwemo Lengo la taasisi, majukumu ya taasisi,watekelezaji wa majukumu na uwajibikaji wa watumishi
Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya ukaguzi Rufaa na malalamiko Bi Asya Mussa Ali amesema Lengo la serikali kuidhinisha miundo mbali na kuimarisha utoaji wa huduma ni kupunguza gharama za uendeshaji kwa taasisi zake.